Saturday, June 3, 2023

NJIA MUHIMU ZA KUWAVUTIA WATEJA

 PART I



Tuangalie baadhi ya njia ambazo zinaweza kutumika ili kuwavuta wateja katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na wajasiriamali. Ikumbukwe njia hizi ni baadhi kati ya nyingi ambazo zinaweza kujenga ufanisi na kuwezesha biashara kusonga mbele.


1. Fanya utafiti wa mahali pazuri pa kufanyia biashara.Eneo ambalo biashara ipo ni jambo la msingi sana katika kuwavutia wateja na kujenga ufanisi katika biashara. Ni vyema pia kutambua si kila biashara inafaa kwa kila eneo na vilevile si kila eneo linafaa kwa kila biashara!

Unaweza kulalamika kwamba biashara sio nzuri na mambo hayaendi lakini kumbe mwanzo wa yote ni biashara yenyewe kutokuwa kwenye eneo sahihi, haya ni makosa yanayofanywa na wajasiriamali wengi hivyo chagua eneo sahihi kwaajili biashara yako. Inawezekana upatikanaji wa maeneo ya biashara hasa maeneo mazuri yanahusisha gharama kubwa katika upatikanaji wake, ni muhimu ufanye tathmini ya uhusiano wa eneo na aina ya biashara unayotegemea kufanya.


2. Tambua wateja halisi wa biashara yako.

Je ni wapita njia? Unapoamua kufanya biashara fikiria pia juu ya walengwa halisi wa biashara husika, ingawa wanaweza kutokea wateja mbalimbali lakini lazima walengwa wawepo.

Elewa wateja ni msingi wa mafanikio katika biashara yako, jiulize wateja wako ni akina nani, nini kitawasukuma kuja kununua kwako, je ni watu wenye uwezo wa kifedha kwa kiasi gani na wanatoka wapi? Ukijiuliza maswali haya utaweza kufahamu namna ya kubuni biashara nzuri kwaajili ya wateja wako.Kwa mfano ukienda benki kuna akaunti za aina mbalimbali kutokana na madaraja ya wateja, kuna akaunti za makampuni, akaunti za watoto n.k. Hivi ndivyo na wewe kama mjasiriamali unatakiwa kufikiria kuhusu aina ya wateja wako.

Ni muhimu kuwa na mchanganuo wa aina mbalimbali za wateja unaowalenga katika bishara yako. Haiwezekani ‘’nguo’’ moja ikamtosha kila mtu! Kwa mfano kama umeamua kufungua duka la nguo jiulize walengwa ni kina nani na utawapataje?Kumbuka soko ni kubwa sana na wateja ni wengi, hivyo wewe kama mjasiriamali unatakiwa kuwaainisha wateja wako katika matabaka kutokana na aidha mila, desturi, uwezo wa kiuchumi, jinsia, elimu, au maeneo wanayotoka.


3. Ainisha bei stahiki ya bidhaa zako.

Ni muhimu kwa mjasiriamali kupanga bei za bidhaa zake kwa namna ambayo itawaridhisha wateja. Pamoja na kuwa na soko la bidhaa zako, yakupasa kuwa na bei zenye kukubalika miongoni mwa wateja wako.Vilevile angalia uwezo wa kiuchumi wa eneo husika, zipo baadhi ya bidhaa ambazo bei zake zinaeleweka na zipo bidhaa ambazo bei zake hutofautiana kutokana na mahali. Hii yote inatokana na uwiano wa kiuchumi, mila, desturi na tamaduni za jamii husika.Kuna changamoto kubwa katika upangaji wa bei za bidhaa, hii ni kwasababu mara nyingi bei huwakilisha aidha gharama za uzalishaji wa bidhaa au thamani ya bidhaa husika. Inashauriwa kuwa ni vyema mjasiriamali asijifunge katika upangaji wa bei za bidhaa zake na badala yake acheze na soko.


SOMOLITAENDELEA

SHARENAMWENZAKOAJIFUNZEPIA

0 comments:

Ad